Maswali ya mara kwa mara
SACCOS NI NINI NA NI UPI UTOFAUTI NA BENKI
JIBU: Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya ushirika na. 6 ya mwaka 2013 sehemu ya kwanza k/f 2. Na sehemu ya pili k/f 3 (1) neno saccos ni kifupi cha neno la kiingereza “savings and credit co-operative society” kiswahili likiwa na maana ya chama cha ushirika wa akiba na mikopo.
Huu ni muunganiko wa hiari kisheria, ambapo watu kwa pamoja wakiwa na lengo la pamoja katika kuanzisha umoja wao wa kifedha, kwa lengo la kuweka akiba na kukopeshana ili kujikwamua katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii na kugawana ziada iliyopatikana kwa kufuata sheria , kanuni na taratibu za vyama vya ushirika na mabadiliko yake.
BENKI: Ni taasisi ya kifedha ambayo muundo wake na taratibu za uendeshwaji wake ni kwa mujibu wa sheria na 12 ya mabenki na taasisi za kifedha ya mwaka 1991 na mabadiliko yake. Mtu yeyote anaweza kuwa na akaunti ya benki inayomuwezesha kuweka pesa na kuchukua wakati wowote. Taasisi hizi zinaendeshwa chini ya usimimamizi wa benki kuu na faida yake ni kwa wenye hisa katika benk hizo.
MWANACHAMA ANASHIRIKISHWAJE KWENYE MAAMUZI
JIBU: Katika uendeshwaji wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo kila mwanachama anayo haki sawa na mwanachama mwingine, pia kila mwanachama anayo haki ya kutoa maoni yake katika vikao /mikutano ya wanachama ya ngazi ya wilaya, mkoa na mkutano mkuu . URA SACCOS katika kila wilaya kuna mwakilishi ambaye ndiye anawakilisha wanachama katika mkutano mkuu kwa kuwasilisha maoni ya wanachama wa wilaya yake, kama ilivyoainishwa katika sheria ya vyama vya Ushirika sehemu ya vi k/f 42, pia katika jedwali la tatu 1 (6) kimeruhusu uwakilishi kutokana na ukubwa na muundo wa chama.
KWA NINI SIJAWAHI KUPATA GAWIWO
.
Gawiwo ni sehemu ya ziada inayopatikana baada ya hesabu za chama kukaguliwa na mkaguzi wa nje na kutoa matengo yote ya kisheria na ziada inayobaki hutolewa maamuzi na Mkutano Mkuu.
Kwa mujibu wa masharti ya chama sehemu ya 9.(e) Mgao huo hufanywa kulingana na hisa anazomiliki mwanachama, ikiwa Chama kinahitaji kukuza mtaji au kuwekeza rasilimali, kiasi hicho cha mgao kitaongezwa kwenye hisa za mwanachama, yaani zitagawiwa hisa za bonas kwa kulingana na hisa alizonazo mwanachama. Hivyo basi chama kimekuwa kikitoa gawiwo kwa kila mwanahisa na kuziongeza katika akaunti ya hisa ya kila mwanachama kwa kila mwaka wa fedha wa chama baada ya hesabu za chama kukaguliwa na kuwasilishwa katika Mkutano Mkuu.
JE NAWEZA KUCHUKUA SEHEMU YA AKIBA ZANGU?
JIBU: kwa mujibu wa sheria ya vyama vya ushirika sehemu ya viii k/f 71 (1) hairuhusu mwanachama kuchukua sehemu ya akiba yake. Kwa kuzingatia kwamba wanachama wake wanaweka akiba kwa viwango na malengo tofauti, Ushirika ukaona ni busara mwanachama aruhusiwe kuchukua sehemu ya akiba yake kwa kuacha kiwango cha Tshs 5,000/= ya kila mwezi kwenye akaunti ya mwanachama na itamlazimu atoe taarifa ya siku tisini.
KWANINI MIKOPO INACHELEWA KWA BAADHI YA WAOMBAJI.
JIBU: Katika suala la utoaji wa mikopo chama kilishafikia azimio la kuwa mikopo yote itatoka ndani ya muda wa siku saba baada ya fomu za mikopo kupokelewa ofisini, hata hivyo kuna baadhi ya waombaji mikopo yao huchelewa kutokana na sababu zifuatazo: –
- Fomu za mkopo kutotumwa kwa wakati Makao Makuu ya URA SACCOS LTD toka zilipopokelewa kwa mwakilishi wa wilaya/mkoa.
- Fomu kutumwa kwa kutokutumia njia isiyo rasmi, na hivyo kuchelewa kufika.
- Baadhi ya fomu zinatumwa zikiwa hazijakamilika/mapungufu kama vile kutokujazwa kwa usahihi, mapungufu ya viambatanisho vinavyotakiwa ambavyo ni kivuli cha kadi ya benki, salary slip halisi, nakala ya kitambulisho cha kazi, fomu kutosainiwa na afisa mhusika ndani ya mkoa au wilaya, fomu kujazwa kiwango kikubwa tofauti na stahili ya mwanachama.
NB: ili kuondoa mapungufu hayo, fomu zote za mikopo zipitie kwa mwakilishi wa eneo husika kwa uhakiki.
MWANACHAMA AKIFARIKI AKIWA NA MKOPO JE AKIBA/HISA ZAKE ZITAFIDIA MKOPO?
Mikopo yote inayotolewa kwa wanachama hukatiwa bima ya maisha, ambapo ikitokea mwanachama amefariki chama hakitachukua akiba/hisa wala mafao ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya marehemu kufidia deni aliloliacha, badala yake deni hilo litafidiwa/kulipwa na mfuko wa Bima ya mkopo.
JE MNAMPANGO GANI KUONGEZA MATAWI MIKOANI
Katika mpango kazi wa Chama wa mwaka 2015- 2017 chama kimejiwekea malengo ya kujenga matawi katika baadhi ya mikoa kulingana na bajeti iliyopangwa na kupitishwa na Mkutano Mkuu, ujenzi wa matawi ni sehemu ya kipaumbele cha chama ambapo hadi sasa ujenzi umekamilika katika Kamisheni ya Polisi Zanzibar na unaendelea katika hatua za mwisho katika mikoa ya Mwanza na Tanga, vilevile ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni katika mikoa ya Dodoma, Mbeya na Kigoma. Lengo la ujenzi huu ni kusogeza huduma kwa wanachama, ambapo huduma zote zitolewazo Makao Makuu zitafanyika katika matawi husika.