URA SACCOS LTD YAPATA MAFUNZO NCHINI KENYA
Katika kuhakikisha kuwa chama kinaendelea kujiimarisha katika kila sekta, Wajumbe wa bodi, kamati ya usimamizi na Menejimenti ya Chama wamepata fursa ya kufanya ziara ya mafunzo jijini Nairobi, lengo likiwa ni kuongeza weledi katika namna bora ya kuwainua kiuchumi watumishi wa Jeshi la Polisi pamoja na familia zao.
Akiongea Jijini Nairobi wakati wa mafunzo hayo Mwenyekiti wa Bodi ya Usalama wa Raia SACCOS Kamishna Polisi wa Utalawa na Menejimenti ya raslimali watu CP Suzan Kaganda amesema kuwa wamejifunza vitu vingi ambavyo vina tija katika uendeshaji wa SACCOS huku akiweka wazi kuwa wanakwenda kuboresha huduma baada ya mafunzo hayo.
CP Kaganda amewapongeza SACCO ya Polisi Nchini Kenya kwa namna ambavyo imeonesha viwango bora katika kutoa huduma kupitia Tehama na kuwa miongoni mwa SACCO bora barani Africa.
Naye David Kagogo ambaye ni Naibu mwenyekiti wa Kenya National Police DT SACCO amewashukuru wajumbe hao kutoka URA SACCOS Tanzania kufika na kujifunza namna ambavyo nchi hiyo inavyofanya kazi katika sekta ya ushirika huku akiwaomba kuyachukua mafunzo hayo kikamilifu ili kuongeza ufanisi na maarifa katika utendaji kazi ndani ya saccos ya Polisi Tanzania.