Habari zote

MATUKIO

Elimu kwa wanachama yafika Tanga, Kinondoni, Kigamboni, Arusha, Igunga na Geita

Kwa kutekeleza msingi wa tano wa ushirika, timu za URA SACCOS zimetoa elimu ya fedha, maandalizi ya kustaafu, matumizi ya URA Mobile na mrejesho wa Mkutano Mkuu.

URASACCOS Admin

Katika kuutekeleza msingi wa tano wa ushirika kwa vitendo, URA SACCOS Ltd imewafikia wanachama wake katika mikoa na wilaya mbalimbali mwezi Machi 2026 na kuwapatia elimu ya ushirika.

Mkoani Tanga, tarehe 19 Machi, wanachama walipata elimu juu ya huduma mbalimbali zitolewazo na chama, umuhimu wake katika kujikwamua kiuchumi na namna ya kuwekeza ndani ya chama, pamoja na maarifa ya fedha katika maandalizi ya kustaafu. Wilayani Kinondoni, timu iliyoongozwa na Meneja wa Tawi la Dar es Salaam, Mrakibu wa Polisi Edwine Mkole, iliwafikia wanachama wa Mabwepande; na wilayani Kigamboni timu iliyoongozwa na Afisa Uhusiano ASP Salimu Mwakasa ilisisitiza kuweka Akiba, Amana na Hisa kupitia mfumo wa kidijitali wa URA Mobile.

Mkoani Arusha, Mwakilishi CPL Chiunda David aliwataka askari wa STPU kuzingatia uwekezaji wa kudumu ikiwemo kununua hisa. Wilayani Igunga na mkoani Geita, watendaji wa Kanda ya Ziwa, INSP Godfrey Pallangyo (Afisa Mikopo) na INSP Heri Mtemaluge (Afisa Tehama), walitoa mrejesho wa maazimio ya Mkutano Mkuu uliofanyika Novemba 2025 mkoani Arusha na masuala yanayotarajiwa kutekelezwa mwaka 2026.

Msisitizo katika vikao vyote ulikuwa nidhamu ya fedha, matumizi ya mifumo ya kidijitali kurahisisha huduma na kuongeza uwazi, pamoja na uelewa wa haki na wajibu wa mwanachama ndani ya chama.

Picha zaidi

Imechapishwa pia kwenye Instagram

Shiriki:
Elimu kwa wanachama yafika Tanga, Kinondoni, Kigamboni, Arusha, Igunga na Geita | URASACCOS