Mashuhuda
Hadithi halisi za wanachama wa URA SACCOS. Kwa miaka 20 (2006 – 2026), mikopo na akiba za chama zimewawezesha wanachama kujenga nyumba, kuanzisha miradi ya ufugaji, kilimo, uvuvi na biashara, na kutoa ajira kwa wengine.

Hussein K. Mdoe - ACP, Dodoma
Nyumba za Kupanga
“URA SACCOS si sehemu ya kupata mikopo tu, bali ni mahali pa kujenga msingi wa uwekezaji na usalama wa kifedha.”
Mimi ni mwanachama wa URA SACCOS tangu mwaka 2006. Katika miaka 20 ya uanachama, URA SACCOS imekuwa nguzo muhimu ya mafanikio yangu ya uwekezaji. Kupitia mikopo niliyopata, nimeweza kununua viwanja na kuendeleza uwekezaji wa nyumba za kupangisha, zinazojulikana kama Mdoe Turning Point, jijini Dodoma. Leo ninatoa huduma ya makazi kwa wafanyakazi wa Serikali na sekta binafsi, kipindi ambacho mahitaji ya nyumba yalikuwa makubwa.
Ninawashauri wanachama wenzangu kuweka akiba kwa bidii na kukopa kwa malengo yaliyo wazi. Kabla ya kuwekeza, ni muhimu kufanya utafiti ili kuhakikisha mkopo unatumika kwenye mradi wenye tija. URA SACCOS ina fursa mbalimbali za kuweka akiba, hivyo tusitegemee mshahara pekee katika kukuza akiba zetu. Kwangu, URA SACCOS si sehemu ya kupata mikopo tu, bali ni mahali pa kujenga msingi wa uwekezaji na usalama wa kifedha. Kupitia chama nimepata mafanikio makubwa, na ninawatia moyo wanachama wenzangu kuitumia fursa hii vizuri.

Happiness S. Ligomola - SGT, Mbeya
Mfugaji wa Kuku
“Ufugaji huu umenufaisha familia yangu, jamii inayonizunguka kwa kutoa fursa za ajira na kuleta maendeleo.”
Nilipohamia Mbeya mwaka 2016, nilipata mkopo wangu wa kwanza wa mshahara kupitia URA SACCOS na kuanzisha banda langu la kwanza la kuku wa mayai. Baadaye, nilipata mikopo ya ujasiriamali iliyoniwezesha kujenga mabanda zaidi na kupanua mradi wangu hatua kwa hatua.
Kilichonivutia URA SACCOS ni riba na masharti nafuu ya muda wa marejesho. Hata mikopo yenye muda wa zaidi ya miezi 12 inaendelea kuwa na riba nafuu. Mwanzoni haikuwa rahisi, kwani kipato changu kilikuwa kidogo na hakikutosheleza mahitaji ya mradi. Hata hivyo, sikuacha. Nilianza na kuku 150, nikafikia 2,000, na sasa nina zaidi ya kuku 7,000 katika mabanda yangu ya hapa nyumbani na shambani.
Mradi huu haujanufaisha familia yangu pekee. Tunawapa vijana fursa za ajira, tunawalipa na kuwawezesha kusaidia familia zao. Vilevile, jamii inayotuzunguka inanufaika kwa kupata mayai kwa urahisi. Kupitia URA SACCOS, nimeweza kukuza biashara yangu, kujenga maisha yangu na kuchangia maendeleo ya wengine.

Abdalla M. Machano - S/SGT, Zanzibar
Mvuvi wa Samaki
“Kupitia fursa hii, nimeweza kujenga nyumba, kugharamia elimu ya watoto wangu na kukidhi mahitaji mengine ya familia.”
Nilijiunga na URA SACCOS mnamo mwaka 2019/2020 na kupata mkopo ambao niliutumia kununua boti la faiba na vifaa vya uvuvi ili kumwezesha mwanangu kupata ajira, kwani wakati huo hakuwa na kazi. Kupitia mkopo huo, tuliweza kuanzisha shughuli za uvuvi na kujenga chanzo cha mapato kwa familia yetu.
Vifaa hivyo vinatuwezesha kufanya uvuvi wa aina mbalimbali, ikiwemo uvuvi wa dagaa na samaki wakubwa kwa kutumia nyavu na mishipi. Tunabadilisha aina ya uvuvi kulingana na fursa na mapato yanayopatikana. Tunapomaliza uvuvi wa usiku wa samaki wakubwa, tunaweza kuendelea na uvuvi wa mchana kwa kutumia mishipi ili kuongeza mapato.
Kwa kweli, URA SACCOS imekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yangu. Kupitia fursa hii, nimeweza kujenga nyumba, kugharamia elimu ya watoto wangu na kukidhi mahitaji mengine ya familia. Ninashukuru kwa mkopo huu, ambao haukunisaidia mimi pekee, bali pia ulimfungulia mwanangu mlango wa ajira na kutuwezesha kusonga mbele kimaisha.

Billya T. Bedson - SGT, Kibaigwa
Mkulima wa Nyanya
“Maisha yangu yalikuwa ya kawaida sana, lakini baada ya kujiunga na kuanza kutumia huduma za URA SACCOS hasa mikopo, maisha yangu yamebadilika kwa kiasi kikubwa.”
Mimi ni mwanachama wa URA SACCOS, nilijiunga na chama mwaka 2009. Baada ya kujiunga na SACCOS niliomba mkopo wangu wa kwanza mwaka 2015. Kwa kuwa mimi nimezaliwa na kukulia kijijini, kilimo kimekuwa ni jambo ninalopenda kufanya, hivyo nilifanya maamuzi ya kutumia mkopo huu kuwekeza kwenye kilimo cha nyanya.
Kabla ya kujiunga na SACCOS, maisha yangu yalikuwa ya kawaida sana, lakini baada ya kujiunga na kuanza kutumia huduma za URA SACCOS hasa mikopo, maisha yangu yamebadilika kwa kiasi kikubwa.
Baada ya kuanzisha mradi huu wa kilimo cha nyanya, niliweza kupata faida iliyoniwezesha kujenga nyumba yangu ya kuishi na kuhama katika nyumba ya kupanga.
Kupitia mradi huu nimeweza kutoa ajira za kudumu kwa vijana watano na za muda mfupi kwa vijana wengi kama vile kupalilia mazao, kuchuma au kupiga dawa ambapo malipo hufanywa kwa siku ili kuwawezesha kujikimu na familia zao.

Frank H. Bukole - Rtd. S/SGT, Dodoma
Vyumba vya Wageni
“Ninawahimiza wanachama wenzangu kuitumia vizuri fursa hii ya uwepo wa URA SACCOS, kuwa na nidhamu na kutumia mikopo kwa tija.”
Nilikuwa miongoni mwa wanachama wa kwanza kujiunga na URA SACCOS. Kabla ya kuanzishwa kwake, askari wengi tulikosa sehemu salama ya kupata mikopo na wakati mwingine tulikopa kwa masharti yaliyotuumiza. URA SACCOS ilipotujia, ilitupa mikopo yenye riba nafuu pamoja na elimu ya ujasiriamali iliyotusaidia kuelewa namna bora ya kutumia mikopo kwa maendeleo.
Kwangu, mchango wa URA SACCOS unaonekana katika maisha ya familia yangu. Nimefanikiwa kuwasomesha watoto wangu wote watatu hadi chuo kikuu, na sasa wana maisha yao. Pia, kupitia mikopo ya ushirika huu, nimejenga nyumba na nyumba za wageni ninazoendesha, pamoja na kumiliki magari yangu. Mafanikio haya yametokana kwa kiasi kikubwa na huduma za URA SACCOS.
Ninawahimiza wanachama wenzangu kuitumia vizuri fursa hii, kuwa na nidhamu na kutumia mikopo kwa tija. Ukiwa na mipango na uvumilivu, URA SACCOS inaweza kuwa chachu ya kubadilisha maisha yako.

