Close

HAFLA YA MAKABIDHIANO VIFAA TIBA VYA MSAADA URASACCOS LTD KWA JESHI LA POLISI

Mkuu wa Jeshi la Polisi akisaini hati ya makbidhiano
Mkuu wa Jeshi la Polisi pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya URA Saccos Ltd wakisaini hati ya makbidhiano wakishuhudiwa na Meneja Mkuu wa URA Saccos Ltd

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchi, IGP. Camillus Wambura amepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 235.5 kutoka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS Ltd) leo Aprili 20,2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi la Polisi Iliyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.

Msaada huo unajumuisha mashine ya x-ray ya kisasa, vifaa vya maabara, vifaa mbalimbali vya mazoezi tiba na vifaa vya wodini vya kulazia wagonjwa vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya Tshs 235,553,90.

Mkuu wa jeshi la Polisi akiwa na mwenyekiti wa Bodi ya URA Saccos Ltd kwenye chumba maalum ilipofungwa mashine ya kisasa ya X-Ray iliyotolewa na URA Saccos Ltd
Mkuu wa jeshi la Polisi akiwa na mwenyekiti wa Bodi ya URA Saccos Ltd kwenye chumba maalum ilipofungwa mashine ya kisasa ya X-Ray iliyotolewa na URA Saccos Ltd

IGP. Wambura amesema vifaa hivyo vimefika wakati muafaka ambapo Jeshi la Polisi lipo katika hatua mbalimbali za maboresho ikiwemo kuhakikisha askari wake wanapata huduma bora za Afya. “Vifaa tiba hivi vitaendelea kusaidia kupanua wigo wa utoaji huduma katika vituo tiba vyetu kwa watumishi wa Jeshi la Polisi, familia zao na wananchi kwa ujumla” alisema afande IGP. Wambura.

Mkuu wa Jeshi la Polisi akipokea hati ya Makabidhiano kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya URA Saccos Ltd
Mkuu wa Jeshi la Polisi akipokea hati ya Makabidhiano kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya URA Saccos Ltd

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya URA SACCOS LTD ambaye pia ni Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu, CP. Suzan Kaganda amesema chama kimekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kutoka na ziada inayopatikana na kuirudisha kwa jamii kama msingi wa Saba wa Ushirika unavyotaka.

CP. Kaganda amesema kuanzia mwaka 2017 ulipoanza utaratibu huo chama hicho cha ushirika kimeshatoa kwa jamii vifaa tiba vyenye thamani zaidi ya Tshs 581,000,000 lengo ni kupunguza changamoto za kitabibu “Ushirika unaamini huduma ya Hospitali sio tu inawanufaisha Askari lakini pia jamii ya watanzania wanaohudumiwa kwenye Hospitali zetu, hivyo kuleta maana halisi ya kurudisha kwa jamii na kuihudumia kupitia vifaa tiba hivyo, alisema CP. Kaganda.

Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Anjela Nalimi ameipongeza URA SACCOS Ltd pia amesema hii iwe ni chachu kwa vyama vingine vya ushirika kuiga mfano huu kwa kutumia sehemu za fedha za ziada kuijali jamii.

Msaada huo wa vifaa tiba unakwenda kutumika katika hospitali ya rufaa ya Kilwa Road na zahanati 6 za Polisi ambazo ni Zahanati ya Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar ES Salaam, Zahanati ya shule ya Polisi Moshi, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Mtwara, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Tanga, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Dodoma na Zahanati ya Polisi Mkoa Kaskazini Pemba.

Picha mbalimbali za matukio: –

Mkuu wa Jeshi la Polisi akipokea hati ya Makabidhiano kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya URA Saccos Ltd